Jumanne, 15 Machi 2016

HADITHI YA MWIZI

HADITHI YA MWIZI
Habari ndugu msomaji wa blog ya “boreshamaisha”. Inawezekana kichwa cha makala hii kimekushitua kidogo. Leo nimetamani sana tujifunze kitu kwa kupitia wezi.
Siku moja nikiwa sokoni sehemu wanapouza nguo za mitumba dada mmoja aliyekua akichagua nguo aliibiwa simu.
Baada ya mwizi kuchukua simu tu, dada yule alishituka na kupiga kelele za mwizi na watu wakaanza kumfukuza mwizi yule kwa hasira huku kila mmoja akijaribu kuokota silaha iliyopo karibu ili amrushie mwizi yule. Lakini cha ajabu ni kwamba mwizi aliweza kuwatoroka watu wote na kupotea vichochoroni.

Naomba uelewe kuwa nia yangu sio kumsifia mwizi kwa kile alichokifanya lakini natamani ujifunze kitu kutoka kwa mwizi huyu.

Kwanza mwizi huyu alijipanga tangu muda mrefu. Yaani aliisoma picha yote ya namna wizi wake utakavyokwenda mpaka atakapofanikiwa.

Pili mwizi huyu alikua na target. Alifahamu tokea mwanzo ni nini alikitaka kutoka kwa nani na akajipanga kukipata. Nadhani mwizi alitumia muda mwingi kutafuta taarifa za dada huyu. Yaani ni aina gani ya simu anayoitumia na akiiweka anaweka wapi na pia saikolojia kidogo ya wakati gani dada huyu anaweza kuwa amejisahau na hivyo kuweza kumwibia kwa urahisi.

Tatu mwizi huyu alikua ni mfuatiliaji wa hali ya juu na hakukata tamaa. Naamini kuwa alianza safari ya kumfuatilia dada huyu kwa muda  na kwa usiri ili dada huyu asijue kuwa alikua akifuatiliwa. Hakukata tamaa ingawa hakufahamu mwisho wa safari ya dada huyu.

Lakini nne mwizi huyu alikua tayari kukabili hatari ya kukamatwa kama asingefanikiwa kuwaponyoka watu wote wale. Lakini bila kujali hatari hiyo bado mwizi huyu alijikita katika kuangali matokeo chanya ambayo kwa namna moja au nyingine yalimpa nguvu za kuweza kufanikisha lengo lake.

Ndugu msomaji, kama kila mmoja wetu angekua na mipango ya namna hii na kutilia umakini kwa kile anachokitaka, na kutafuta mbinu mbali mbali za kufikia lengo alilojiwekea kama mwizi huyu alivyofanya nadhani malengo yetu mengi tungeyafikia.

 Unaweza kuwaza kuwa sio kila mara ukiweka juhudi utafanikiwa, ni kweli sio kila mara lakini mara nyingi ukiweka juhudi unafanikiwa. Na mara zote kama huwezi kujaribu huwezi kufanikiwa. Uamuzi ni wako kuona kama unaweza kujitoa kwa kuweka juhudi katika lengo ulilonalo au kuacha ili usubiri matokeo hasi.
MWANDISHI:             ESTHER NGULWA
MAWASILIANO:      0767 900 110/ 0714 900 110
                             estherngulwa87@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni