Jumatatu, 3 Aprili 2017

Huyu Ndiye Mtu Anayeweza Kukusaidia Kutatua Changamoto Unazozipitia.



Huyu Ndiye Mtu Anayeweza Kukusaidia Kutatua Changamoto Unazozipitia.
Mara nyingi binadamu tumekuwa tukilalamika kuhusu ugumu wa maisha na changamoto kuzidi kuongezeka kadiri siku zinavyozidi kwenda. Katika jamii zetu kuomba msaada ni jambo jema kabisa lakini tunachozingatia ni wapi au kwa mtu wa aina gani tunaomba msaada. Kwa wale wenye imani katika dini kila mmoja na dini yake huomba ili aweze kupata unafuu juu ya changamoto zinazomkabili.

Lakini hii haimaanishi kuwa changamoto zinakwisha, ukivuka changamoto moja bado inakuja nyingine na nyingine hivyo hivyo, ilimradi maisha hayaishi changamoto. Na hii hutokea kwa watu wenye vipato vikubwa na vidogo, rika tofauti tofauti kwa ufupi kila mmoja bila kujali hadhi,muonekano au uwezo wake alionao changamoto humkabili.

Wakati huu huwa mgumu lakini ugumu huu hutegemea aina ya mtu aliyepata changamoto. Kuna wengine wanaweza kupata changamoto ndogo na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzihimili lakini wengine wakawa na changamoto ndogo lakini wakashindwa kuzikabili. 

Ukubwa au dogo wa changamoto hutegemeana na hali ya upokeaji wa changamoto husika kwa yule alipatwa na changamoto hiyo. Katika hali ya kawaida hakuna kipimo cha kuonesha kuwa changamoto za aina Fulani ni ngumu kuliko za aina nyingine, inategemea sana na aina ya mtu na muda changamoto hiyo inapotokea.

Mara nyingi tunapokumbwa na mitihani hii ya maisha huwa tunatamani tupate mfariji kama nilivyoelezea kwenye sehemu ya kwanza hapo juu. Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anayeweza kutusaidia kutatua changamoto tulizonazo bali kitu tunachoweza kukipata ni ushauri ambao baadae wewe binafsi utachagua ni maamuzi gani unahitaji kuyafanya.(Soma pia http://boreshamaisha.blogspot.com/2016/03/hadithi-ya-mwizi.html)

Kuomba ushauri ni jambo jema hutusaidia sana kupunguza msongo wa mawazo kutokana na mitihani tunayopitia lakini kufikiri kuwa kuna mtu atakupa mbinu zitakazo kuhakikishia mafanikio sio rahisi. Unaweza kupata uzoefu wa namna mtu mwingine anavyokabili changamoto inayofana na yakwako lakini ukipata uzoefu huo inabidi utambue kuwa wewe pia ni mtu tofauti na uwe mbunifu wa kutumia uzoefu uliopewa vizuri ili kuweka mambo yako sawa. Hata kama utatamani kutatua kwa njia ya imani ya dini yako bado kuna hatua za kawaida kama binadamu utatakiwa kuzichukua ikiwa ni kufanya maamuzi ambayo yataleta mabadiliko katika hali unayopitia.

Kwa hiyo mtu anayeweza kutatua changamoto unayopitia ni wewe mwenyewe, na hao wanaokuzunguka watakupa msaada wa mawazo tu, kwani hata wao wanachangamoto zao. Utulivu, hekima na busara ni mambo muhimu sana katika kufanya maamuzi sahihi.

Mwandishi: Esther Ngulwa
Barua Pepe: estherngulwa87@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni