Jumatatu, 3 Aprili 2017

Huyu Ndiye Mtu Anayeweza Kukusaidia Kutatua Changamoto Unazozipitia.



Huyu Ndiye Mtu Anayeweza Kukusaidia Kutatua Changamoto Unazozipitia.
Mara nyingi binadamu tumekuwa tukilalamika kuhusu ugumu wa maisha na changamoto kuzidi kuongezeka kadiri siku zinavyozidi kwenda. Katika jamii zetu kuomba msaada ni jambo jema kabisa lakini tunachozingatia ni wapi au kwa mtu wa aina gani tunaomba msaada. Kwa wale wenye imani katika dini kila mmoja na dini yake huomba ili aweze kupata unafuu juu ya changamoto zinazomkabili.

Lakini hii haimaanishi kuwa changamoto zinakwisha, ukivuka changamoto moja bado inakuja nyingine na nyingine hivyo hivyo, ilimradi maisha hayaishi changamoto. Na hii hutokea kwa watu wenye vipato vikubwa na vidogo, rika tofauti tofauti kwa ufupi kila mmoja bila kujali hadhi,muonekano au uwezo wake alionao changamoto humkabili.

Wakati huu huwa mgumu lakini ugumu huu hutegemea aina ya mtu aliyepata changamoto. Kuna wengine wanaweza kupata changamoto ndogo na kuwa na uwezo mkubwa wa kuzihimili lakini wengine wakawa na changamoto ndogo lakini wakashindwa kuzikabili. 

Ukubwa au dogo wa changamoto hutegemeana na hali ya upokeaji wa changamoto husika kwa yule alipatwa na changamoto hiyo. Katika hali ya kawaida hakuna kipimo cha kuonesha kuwa changamoto za aina Fulani ni ngumu kuliko za aina nyingine, inategemea sana na aina ya mtu na muda changamoto hiyo inapotokea.

Mara nyingi tunapokumbwa na mitihani hii ya maisha huwa tunatamani tupate mfariji kama nilivyoelezea kwenye sehemu ya kwanza hapo juu. Lakini ukweli ni kwamba hakuna mtu anayeweza kutusaidia kutatua changamoto tulizonazo bali kitu tunachoweza kukipata ni ushauri ambao baadae wewe binafsi utachagua ni maamuzi gani unahitaji kuyafanya.(Soma pia http://boreshamaisha.blogspot.com/2016/03/hadithi-ya-mwizi.html)

Kuomba ushauri ni jambo jema hutusaidia sana kupunguza msongo wa mawazo kutokana na mitihani tunayopitia lakini kufikiri kuwa kuna mtu atakupa mbinu zitakazo kuhakikishia mafanikio sio rahisi. Unaweza kupata uzoefu wa namna mtu mwingine anavyokabili changamoto inayofana na yakwako lakini ukipata uzoefu huo inabidi utambue kuwa wewe pia ni mtu tofauti na uwe mbunifu wa kutumia uzoefu uliopewa vizuri ili kuweka mambo yako sawa. Hata kama utatamani kutatua kwa njia ya imani ya dini yako bado kuna hatua za kawaida kama binadamu utatakiwa kuzichukua ikiwa ni kufanya maamuzi ambayo yataleta mabadiliko katika hali unayopitia.

Kwa hiyo mtu anayeweza kutatua changamoto unayopitia ni wewe mwenyewe, na hao wanaokuzunguka watakupa msaada wa mawazo tu, kwani hata wao wanachangamoto zao. Utulivu, hekima na busara ni mambo muhimu sana katika kufanya maamuzi sahihi.

Mwandishi: Esther Ngulwa
Barua Pepe: estherngulwa87@gmail.com

Jumanne, 15 Machi 2016

HADITHI YA MWIZI

HADITHI YA MWIZI
Habari ndugu msomaji wa blog ya “boreshamaisha”. Inawezekana kichwa cha makala hii kimekushitua kidogo. Leo nimetamani sana tujifunze kitu kwa kupitia wezi.
Siku moja nikiwa sokoni sehemu wanapouza nguo za mitumba dada mmoja aliyekua akichagua nguo aliibiwa simu.
Baada ya mwizi kuchukua simu tu, dada yule alishituka na kupiga kelele za mwizi na watu wakaanza kumfukuza mwizi yule kwa hasira huku kila mmoja akijaribu kuokota silaha iliyopo karibu ili amrushie mwizi yule. Lakini cha ajabu ni kwamba mwizi aliweza kuwatoroka watu wote na kupotea vichochoroni.

Naomba uelewe kuwa nia yangu sio kumsifia mwizi kwa kile alichokifanya lakini natamani ujifunze kitu kutoka kwa mwizi huyu.

Kwanza mwizi huyu alijipanga tangu muda mrefu. Yaani aliisoma picha yote ya namna wizi wake utakavyokwenda mpaka atakapofanikiwa.

Pili mwizi huyu alikua na target. Alifahamu tokea mwanzo ni nini alikitaka kutoka kwa nani na akajipanga kukipata. Nadhani mwizi alitumia muda mwingi kutafuta taarifa za dada huyu. Yaani ni aina gani ya simu anayoitumia na akiiweka anaweka wapi na pia saikolojia kidogo ya wakati gani dada huyu anaweza kuwa amejisahau na hivyo kuweza kumwibia kwa urahisi.

Tatu mwizi huyu alikua ni mfuatiliaji wa hali ya juu na hakukata tamaa. Naamini kuwa alianza safari ya kumfuatilia dada huyu kwa muda  na kwa usiri ili dada huyu asijue kuwa alikua akifuatiliwa. Hakukata tamaa ingawa hakufahamu mwisho wa safari ya dada huyu.

Lakini nne mwizi huyu alikua tayari kukabili hatari ya kukamatwa kama asingefanikiwa kuwaponyoka watu wote wale. Lakini bila kujali hatari hiyo bado mwizi huyu alijikita katika kuangali matokeo chanya ambayo kwa namna moja au nyingine yalimpa nguvu za kuweza kufanikisha lengo lake.

Ndugu msomaji, kama kila mmoja wetu angekua na mipango ya namna hii na kutilia umakini kwa kile anachokitaka, na kutafuta mbinu mbali mbali za kufikia lengo alilojiwekea kama mwizi huyu alivyofanya nadhani malengo yetu mengi tungeyafikia.

 Unaweza kuwaza kuwa sio kila mara ukiweka juhudi utafanikiwa, ni kweli sio kila mara lakini mara nyingi ukiweka juhudi unafanikiwa. Na mara zote kama huwezi kujaribu huwezi kufanikiwa. Uamuzi ni wako kuona kama unaweza kujitoa kwa kuweka juhudi katika lengo ulilonalo au kuacha ili usubiri matokeo hasi.
MWANDISHI:             ESTHER NGULWA
MAWASILIANO:      0767 900 110/ 0714 900 110
                             estherngulwa87@gmail.com

Alhamisi, 6 Agosti 2015

Unaweza Kuwa Vile Unavyotaka Uamuzi Ni Wako

Mara nyingi tumekuwa tukitamani kuwa watu wa aina fulani. Wakati mwingine tumetamani kuwa kama baadhi ya watu wenye mafanikio ambao wanatuvutia sana. 
Lakini wengi wetu tunaishia kutamani tu bila kufikia pale tunapokusudia. Mara kwa mara tumeaminishwa kuwa watu wanaofikia mafanikio wamezaliwa na bahati, au wengi hutumia usemi wa Kiswahili kuwa “maji hufuata mkondo”. Wakiwa na maana kuwa kuna baadhi ya watu au familia ambazo wamejaliwa kuwa na mafanikio na wengine hawawezi kwakua hawana bahati hiyo.


Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu anaweza kufikia kiwango chochote kile cha mafanikio kama akiamua. Kuna baadhi ya kanuni ambazo zinatakiwa kufuatwa ili kufikia popote unapohitaji bila kujali rangi, kimo, kabila, ukoo wala taifa. Kama ambavyo ukifuata kanuni za kushindwa basi lazima utafikia kushindwa bila kujalisha wewe ni nani na unatokea wapi?
Katika kila kiwango unachotaka kufikia, ni vizuri kufahamu kanuni na sheria za kukufikisha eneo hilo. Ukifahamu ni kanuni gani unatakiwa uzifuate, na sheria ambazo unatakiwa kuzizingatia lazima utafika tu pale unapohitaji. Hakuna uchawi wala bahati yoyote ile. Kama ni bahati basi anza leo kujifunza kuhusu kanuni hizo na sheria hizo na uzifuate ili ujitengenezee bahati mwenyewe.
Kuna uzuri wa kutengeneza bahati yako mwenyewe kuliko kubahatika katika bahati nasibu ambazo unajaribu bila kuwa na uhakika kama wewe ndiye utakayebahatika au la. Unapojibahatisha mwenyewe unakua umejiandaa kupokea matokeo ambayo umekusudia yatatokea na ikiwa kama ulivyopanga inakuwa rahisi kulinda na kuongeza mafanikio yale ili uende kiwango cha juu zaidi. Tofauti na bahati nasibu ambazo mara nyingi ukishabahatika unachanganyikiwa kwa sababu ni kitu ambacho kimekuja kwa kushtukiza tu. Kukikuza pia ni kazi ngumu kwa sababu sio wewe uliyekitafuta. Simaanishi kuwa hutakiwi kupata bahati nasibu, maana yangu ni kwamba huwezi kujenga maisha unayoyataka kwa kutegemea kua kuna siku utabahatika na baada ya kufanya hivyo basi ndoto zako zitatimia.
Ili uweze kufikia kiwango cha mafanikio unachohitaji ni muhimu sana kuwa na nidhamu binafsi. Kama maisha yangekuwa ni aina fulani ya mlo mzuri, basi ningeweza kusema kuwa nidhamu ni kiungo muhimu sana ambacho kinafanya chakula hicho kiwe na ladha hiyo tamu. Ni vigumu sana kupanga shughuli na kuitimiza kwa wakati kama hauna nidhamu binafsi. Unaweza kujikuta hata kuchaji simu tu huwezi na unalalamika kuwa umeishiwa chaji umeme ukikatika na simu ulikua nayo muda wote na muda wote huo ulikua unawaza kuichaji , lakini kwa kutokua na nidhamu binafsi umejikuta unaendelea na mambo mengine yasiyo ya muhimu zaidi kwa wakati huo na kuacha kufanya mambo ya muhimu. Huu ni mfano mdogo tu wa namna ambavyo watu wengi wanashindwa kuwa na nidhamu katika maisha ya kila siku.
Ukisoma makala hizi, nakusihi jitahidi kuzipa nafasi katika akili yako ili uweze kukumbuka. Wakati hali ya kujisahaulisha, uvivu na kuahirisha vinapokuandama jitahidi ukumbuke baadhi ya vipengele ambavyo vitakusaidia kukupa nguvu ya kufanya shughuli ulizopangilia ambazo zitakusaidia kufikia kiwango cha mafanikio unachohitaji.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA 
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110 
Whatsaap: 0652 025244 
Facebook 

Mambo Nane(8) Yatakayokufanya Uwe Na Fikra Chanya Kila Wakati Ili Uweze Kufikia Mafanikio

Habari ndugu msomaji. Leo ningependa tuangalie namna ambavyo unaweza kujijenga na kuwa na fikra chanya kila wakati bila kujali watu wanaokuzunguka au matukio ambayo yametokea na kukuvunja moyo.
Siri ya kuwa na mafanikio katika kila unalolifanya ni kuwa na fikra chanya. Ukishakuwa na fikra hasi tu, basi hata kukamilisha matamanio yako itakuwa ngumu. Ni dhahiri kuwa vile tunavyoviona nje vilianzia ndani yetu. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana kujenga fikra chanya ili kuleta matokeo mazuri ya nje/katika ulimwengu wa mwili. 


Tutaangalia baadhi ya vitu vitakavyotusaidia kutujengea fikra chanya na kama utakua na baadhi ya sababu ambazo unahisi kwako ni muhimu katika kukuongezea fikra chanya basi utaongezea na uweke katika karatasi ili kila ukiamka uzipitie, ili hali yoyote ile mbaya inapokukumba ukumbuke kuwa kuna mahala unaweza kusoma na ukarudi katika hali yako ya kawaida.
1. Kuamka mapema
Ili siku yako iende vizuri na uwe na fikra chanya ni lazima uamke mapema asubuhi. Ni vizuri kama utaamka saa kumi na moja. Muda wa alfajiri unakupa nafasi ya kupangilia mambo yako vizuri. Kama wewe ni mfanyakazi basi mpaka muda wa kwenda kazini unapofika unakua umekamilisha majukumu yako vizuri na hisia za kukimbizana kwa kuhofia kuwa utachelewa zinakuwa hazipo hivyo kukupa utulivu na hisia chanya kila wakati. Utulivu huu wa akili utakusaidia kuongeza thamani katika kile unachofanya
2. Kuwa na furaha
Jambo jingine la muhimu ni kuwa na furaha. Kufurahia siku yako, ratiba yako ya siku usiione kama adhabu kwako. Kuwafurahia wale wanaokuzunguka na zaidi ya yote ni kujikubali mwenyewe. Ni muhimu kufanya hivyo kwakua kama utafanya kinyume na haya utaishia kuwa na siku, wiki, mwezi na mwaka mbaya kila wakati.
3. Kukamilisha majukumu kwa wakati.
Jambo jingine muhimu ni kukamilisha majukumu yako kwa wakati. Kuna muda unaandika majukumu unayotakiwa kuyafanya lakini unajikuta kwenye shida ya kuahirisha na kuona kesho au baadaye utakuwa na muda wa kufanya shughuli ile. Tatizo ni kwamba kama hujamaliza majukumu hata ukipumzika, haupumziki kwa amani kwakua unakuwa na mawazo ya kutokamilisha lile ulilopanga. Hivyo unajikuta ukiwa na hisia mbaya na kushindwa kufanya hata shughuli nyingine. Hata kama unajisikia uvivu kiasi gani, jitahidi uanze kufanya kazi yako na kuimaliza kwa wakati. Itakupa hamasa ya kufanya mambo mengine pia utapata raha ya kupumzika na kutumia muda na wale uwapendao.
4. Kuepuka masengenyo na majungu.
Unapokuwa unajihusisha na majungu na masengenyo ni vigumu kuwa na fikra chanya. Kila unachokiona utakiona tofauti kwa kuwa akili yako imekaa katika utayari wa kubeza na kuchambua vibaya kila wakati. 
5. Kulala muda wa kutosha
Tunakuwa na majukumu mengi sana kwa siku. Majukumu hayo yanatufanya tuwe na mawazo mengi sana na hivyo kuifanya akili na mwili kuchoka. Mojawapo ya vitu vinavyosababisha fikra hasi ni kuwa na uchovu na kuona kama maisha ni adhabu, majukumu ni kama utumwa na hivyo kuifanya akili kuchoka zaidi. Ni vizuri kupata muda wa kulala wa kutosha ili kuwezesha akili na mwili kupumzika na ukiamka unaanza siku ukiwa na nguvu mpya ya akili na mwili pia.
6. Kupata muda wa kujipongeza
Mara nyingi tumekuwa tukitamani kupongezwa na watu wengine pale tunapofanya mambo mazuri. Ni jambo zuri ,lakini tumesahau kujipongeza wenyewe kwa kukamilisha majukumu yetu ya kila siku. Unapojipongeza unajihamasisha kukamilisha mambo mengine uliyojipangia. Unapojiahidi zawadi baada ya kutimiza jambo fulani unajipa hamasa ya kuzingatia kile unachokifanya. Hivyo unapata hisia chanya katika kukamilisha yale uliyojipangia.
7. Kuandika majukumu yako kwa siku na kuyafanya kwa kuzingatia muda.
Watu wengi katika ulimwengu huu tumekuwa na shughuli nyingi za kufanya kiasi kwamba unaweza kuchanganyikiwa kama ukiziorodhesha kichwani tu. Mojawapo ya njia ya kupunguza lundo la shughuli kichwani ni kuziweka katika karatasi. Andika shughuli zako katika karatasi na toa kiasi cha muda kwa kila shughuli iliyopo mbele yako. Kwa kufanya hivyo akili inakuwa katika nafasi nzuri ya kutulia na kukamilisha jukumu lililopo badala ya kufikiria juu ya shughuli ambazo bado hazijakamilika.
8. Kutotenda kinyume na imani zako/misingi yako binafsi
Kila mmoja ana imani au misingi yake binafsi ambayo ndiyo huwa chanzo cha maamuzi na matendo yake ya kila siku. Ni vizuri kufahamu ni nini misingi yako binafsi na kuisimamia ili kukufanya ujisikie vizuri kila wakati. Kama utatenda kinyume na misingi yako kwa sababu ya ushawishi wa rafiki au kikundi fulani cha watu basi lazima baada ya muda utahisi vibaya. Sio vizuri kujisaliti wewe mwenyewe kwa kufanya kinyume na vile unavyoamini kwa sababu ya msukumo kutoka kwa wengine au sababu nyingine yoyote ile.
Ni imani yangu kuwa mambo hayo yatasaidia kwa namna moja au nyingine kukujengea fikra chanya. Kumbuka kuwa fikra au hisia au mawazo huleta matokeo ya nini tufanye na vile tunavyovifanya pia hutuletea matokeo ya namna tukavyohisi/kufikiri.
Mwandishi: esther ngulwa
Mawasiliano: 0767 900 110 / 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com
Facebook 

Jumanne, 14 Aprili 2015

Hivi ndivyo Unavyoweza Kujijengea Ujasiri na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Y a Unavyoweza Kufikiri

Hivi ndivyo Unavyoweza Kujijengea Ujasiri na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Y a Unavyoweza Kufikiri
Nina imani umeshawahi kusikia au kusoma historia za watu tofauti tofauti na mara nyingine ukawaza kuwa watu hao walikua jasiri sana. Kuna watu mbalimbali waliowahi kuendesha nchi, kufanya vitu vya utofauti ambavyo kwa hali ya kawaida sio kila mtu anaweza kufanya, watu waliochukua maamuzi magumu ambayo sio rahisi kufikiria kwanini waliamua kuchukua maamuzi magumu kiasi hicho. Inawezekana wakati wanafanya maamuzi hayo hata watu wa karibu yao yaani ndugu na marafiki hawakuungana nao kwakua maamuzi hayo yalikuwa ni magumu mno, hivyo waliwakataza kufanya maamuzi hayo. Ukiwasoma au kuwasikia watu hawa unakubali kuwa watu hawa walikuwa na ujasiri mno.
Inawezekana pia kwenye familia yako kuna mtu jasiri wa namna hii katika eneo fulani la maisha,je na wewe pia ungetamani kuwa  jasiri? Endelea kusoma makala hii mpaka mwisho na ufanyie kazi yale unayoyasoma kwa umakini ili uweze kuwa na ujasiri wa kufanya jambo lolote unalodhani ni zuri na litakuwezesha wewe kukamilisha ndoto za maisha yako.

Nimeorodhesha vitu hivi katika namba lakini haina maana kuwa kitu namba moja ndio cha muhimu zaidi kuliko namba ya mwisho. Vyote ni muhimu kulingana na nini unahitaji.
1.       Weka malengo.
Nina imani sio mara ya kwanza unasoma kitu kama hiki. Mara nyingi umesoma na kusikia watu wakikuambia uweke malengo ya maisha yako. Malengo ya muda mrefu, malengo ya muda wa kati na malengo ya muda mfupi.
Kwanini kuweka malengo kunasaidia kukupa ujasiri?
Ukiorodhesha malengo yako unakuwa unafahamu ni nini unatakiwa ufanye, au njia gani uanatakiwa upite ili kufanikisha lile ulilokusudia katika maisha yako. Na katika kutimiza malengo kuna wakati unatakiwa kufanya maamuzi magumu ambayo yatakuhitaji wewe kuwa na ujasiri ndani yako ili kuweza kuyafanya maamuzi hayo.Fanya  maamuzi hayo na utimize lengo ulilokusudia .Kwa kufanya hivi utakuwa unajijengea ujasiri wa kufanya mambo mengine yaliyopo mbele yako hata kama ni makubwa kiasi gani.
2.       F anya jambo moja baada ya jingine.
Ili uweze kuwa jasiri ni vizuri ufanye jambo moja kwa wakati.kufanya jambo moja kwa wakati  kunakupa urahisi wa kutafuta mbinu za kuweza kufanya jambo hilo. Ukiwa na mambo mengi kichwani unayohitaji kuyafanya na hauna mpangilio ufanye lipi kwanza, unaweza kufikia hatua ukachanganyikiwa na kuamua usifanye jambo lolote lile.
Unaona tu mbele yako kuna mambo mengi na wingi huo wa vitu vya kufanya unaweza kukuondolea ujasiri wa kukamilisha hata jambo moja. Ni vizuri kuandika katika karatasi unahitaji kufanya nini na uweke vitu hivyo katika vipaumbele kuwa unaanza na kipi na utafuatia kipi. Ukifanya vitu vyote kwa wakati mmoja utashindwa kukamilisha vyote, utajiona huwezi kufanya lolote na hivyo kukuondolea hata uthubutu kidogo ulipo ndani yako.
3.       Pata taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya.
Ni vizuri kupata taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya ili upate ujasiri wa kufanya kitu hicho. Inawezekana kweli kitu unachotaka kukifanya kikawa ni kigumu, ukiwa na taarifa hizo unajiandaa tangu mwanzoni kwaajili ya kupambana na ugumu huo. Unatengeneza njia za kupana na ugumu huo. Unapata ujasiri wa kuendelea na lengo lako hata kama mabo yatakuwa magumu kwakua unafahamu kuwa ili kufanikisha lengo lako kunaugumu fulani inabidi uupitie. Hiyo inakupa ujasiri wa kupambana hadi kukamilisha kusudio lako.
Ukiwa hauna taarifa za kutosha juu ya kitu unachoenda kufanya, ukipata changamoto hata kama ndogo, au hata watu wakikukatisha tama, ni rahisi kuacha kufanya jambo ulilotaka kulifanya nakujiona huwezi kufanya jambo lolote kubwa katika maisha yako.
4.       Maandalizi.
Ili kupata ujasiri wa kufanya jambo lolote lililopo mbele yako ni lazima kufanya maandalizi mapema.
Ukiwa na taarifa sahihi za kitu unachokwenda kukifanya ni rahisi kujua ni nini utahitaji, iwe ni vifaa au tabia fulani. Kwa mfano unahitaji kuwa mkulima mzuri wa kahawa na umepata raarifa sahihi kuhusu eneo kahawa zinapostawi, mtaji wake, soko na  faida. Lakini pia umepata taarifa ni nini changamoto katika ulimaji wa kahawa. Basi maandalizi ya kutafuta eneo, mbegu, watu watakao kusaidida, jinsi ya kupambana na changamoto ulizoambiwa hufuatia. Kwa kufanya hivi unapata ujasiri wa kuendelea na kilimo chako huku ukitegemea matokeo mazuri mbeleni.
Asante sana kwa kuungangana nami katika makala hii ya leo. Tutaendelea kuangalia  vitu vingine vitakavyokusaidia kujenga ujasiri wiki ijayo siku kama ya leo.
Nakutakia maisha yenye furaha.

kwa makala nyingine bofya hapa.


MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO:
                           0767 900 110/ 0714 900 110
                             estherngulwa87@gmail.com
                          Facebook
5.