Hivi ndivyo Unavyoweza Kujijengea Ujasiri na Kufanya Mambo Makubwa Zaidi Y a Unavyoweza Kufikiri
Nina imani umeshawahi kusikia au
kusoma historia za watu tofauti tofauti na mara nyingine ukawaza kuwa watu hao
walikua jasiri sana. Kuna watu mbalimbali waliowahi kuendesha nchi, kufanya
vitu vya utofauti ambavyo kwa hali ya kawaida sio kila mtu anaweza kufanya,
watu waliochukua maamuzi magumu ambayo sio rahisi kufikiria kwanini waliamua
kuchukua maamuzi magumu kiasi hicho. Inawezekana wakati wanafanya maamuzi hayo
hata watu wa karibu yao yaani ndugu na marafiki hawakuungana nao kwakua maamuzi
hayo yalikuwa ni magumu mno, hivyo waliwakataza kufanya maamuzi hayo. Ukiwasoma
au kuwasikia watu hawa unakubali kuwa watu hawa walikuwa na ujasiri mno.
Inawezekana pia kwenye familia
yako kuna mtu jasiri wa namna hii katika eneo fulani la maisha,je na wewe pia
ungetamani kuwa jasiri? Endelea kusoma
makala hii mpaka mwisho na ufanyie kazi yale unayoyasoma kwa umakini ili uweze
kuwa na ujasiri wa kufanya jambo lolote unalodhani ni zuri na litakuwezesha
wewe kukamilisha ndoto za maisha yako.
Nimeorodhesha vitu hivi katika
namba lakini haina maana kuwa kitu namba moja ndio cha muhimu zaidi kuliko
namba ya mwisho. Vyote ni muhimu kulingana na nini unahitaji.
1. Weka
malengo.
Nina imani sio
mara ya kwanza unasoma kitu kama hiki. Mara nyingi umesoma na kusikia watu
wakikuambia uweke malengo ya maisha yako. Malengo ya muda mrefu, malengo ya
muda wa kati na malengo ya muda mfupi.
Kwanini
kuweka malengo kunasaidia kukupa ujasiri?
Ukiorodhesha
malengo yako unakuwa unafahamu ni nini unatakiwa ufanye, au njia gani
uanatakiwa upite ili kufanikisha lile ulilokusudia katika maisha yako. Na
katika kutimiza malengo kuna wakati unatakiwa kufanya maamuzi magumu ambayo
yatakuhitaji wewe kuwa na ujasiri ndani yako ili kuweza kuyafanya maamuzi hayo.Fanya maamuzi hayo na utimize lengo ulilokusudia .Kwa
kufanya hivi utakuwa unajijengea ujasiri wa kufanya mambo mengine yaliyopo
mbele yako hata kama ni makubwa kiasi gani.
2. F
anya jambo moja baada ya jingine.
Ili uweze kuwa
jasiri ni vizuri ufanye jambo moja kwa wakati.kufanya jambo moja kwa wakati kunakupa urahisi wa kutafuta mbinu za kuweza
kufanya jambo hilo. Ukiwa na mambo mengi kichwani unayohitaji kuyafanya na
hauna mpangilio ufanye lipi kwanza, unaweza kufikia hatua ukachanganyikiwa na
kuamua usifanye jambo lolote lile.
Unaona tu mbele
yako kuna mambo mengi na wingi huo wa vitu vya kufanya unaweza kukuondolea
ujasiri wa kukamilisha hata jambo moja. Ni vizuri kuandika katika karatasi
unahitaji kufanya nini na uweke vitu hivyo katika vipaumbele kuwa unaanza na
kipi na utafuatia kipi. Ukifanya vitu vyote kwa wakati mmoja utashindwa
kukamilisha vyote, utajiona huwezi kufanya lolote na hivyo kukuondolea hata uthubutu
kidogo ulipo ndani yako.
3. Pata
taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya.
Ni vizuri kupata
taarifa sahihi za kitu unachotaka kukifanya ili upate ujasiri wa kufanya kitu
hicho. Inawezekana kweli kitu unachotaka kukifanya kikawa ni kigumu, ukiwa na
taarifa hizo unajiandaa tangu mwanzoni kwaajili ya kupambana na ugumu huo.
Unatengeneza njia za kupana na ugumu huo. Unapata ujasiri wa kuendelea na lengo
lako hata kama mabo yatakuwa magumu kwakua unafahamu kuwa ili kufanikisha lengo
lako kunaugumu fulani inabidi uupitie. Hiyo inakupa ujasiri wa kupambana hadi
kukamilisha kusudio lako.
Ukiwa hauna
taarifa za kutosha juu ya kitu unachoenda kufanya, ukipata changamoto hata kama
ndogo, au hata watu wakikukatisha tama, ni rahisi kuacha kufanya jambo
ulilotaka kulifanya nakujiona huwezi kufanya jambo lolote kubwa katika maisha
yako.
4. Maandalizi.
Ili kupata
ujasiri wa kufanya jambo lolote lililopo mbele yako ni lazima kufanya
maandalizi mapema.
Ukiwa na taarifa
sahihi za kitu unachokwenda kukifanya ni rahisi kujua ni nini utahitaji, iwe ni
vifaa au tabia fulani. Kwa mfano unahitaji kuwa mkulima mzuri wa kahawa na
umepata raarifa sahihi kuhusu eneo kahawa zinapostawi, mtaji wake, soko na faida. Lakini pia umepata taarifa ni nini
changamoto katika ulimaji wa kahawa. Basi maandalizi ya kutafuta eneo, mbegu,
watu watakao kusaidida, jinsi ya kupambana na changamoto ulizoambiwa hufuatia.
Kwa kufanya hivi unapata ujasiri wa kuendelea na kilimo chako huku ukitegemea
matokeo mazuri mbeleni.
Asante sana kwa kuungangana nami
katika makala hii ya leo. Tutaendelea kuangalia
vitu vingine vitakavyokusaidia kujenga ujasiri wiki ijayo siku kama ya
leo.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA
MAWASILIANO:
0767 900 110/ 0714 900 110
estherngulwa87@gmail.com
Facebook
5.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni