Alhamisi, 6 Agosti 2015

Unaweza Kuwa Vile Unavyotaka Uamuzi Ni Wako

Mara nyingi tumekuwa tukitamani kuwa watu wa aina fulani. Wakati mwingine tumetamani kuwa kama baadhi ya watu wenye mafanikio ambao wanatuvutia sana. 
Lakini wengi wetu tunaishia kutamani tu bila kufikia pale tunapokusudia. Mara kwa mara tumeaminishwa kuwa watu wanaofikia mafanikio wamezaliwa na bahati, au wengi hutumia usemi wa Kiswahili kuwa “maji hufuata mkondo”. Wakiwa na maana kuwa kuna baadhi ya watu au familia ambazo wamejaliwa kuwa na mafanikio na wengine hawawezi kwakua hawana bahati hiyo.


Ukweli ni kwamba kila mmoja wetu anaweza kufikia kiwango chochote kile cha mafanikio kama akiamua. Kuna baadhi ya kanuni ambazo zinatakiwa kufuatwa ili kufikia popote unapohitaji bila kujali rangi, kimo, kabila, ukoo wala taifa. Kama ambavyo ukifuata kanuni za kushindwa basi lazima utafikia kushindwa bila kujalisha wewe ni nani na unatokea wapi?
Katika kila kiwango unachotaka kufikia, ni vizuri kufahamu kanuni na sheria za kukufikisha eneo hilo. Ukifahamu ni kanuni gani unatakiwa uzifuate, na sheria ambazo unatakiwa kuzizingatia lazima utafika tu pale unapohitaji. Hakuna uchawi wala bahati yoyote ile. Kama ni bahati basi anza leo kujifunza kuhusu kanuni hizo na sheria hizo na uzifuate ili ujitengenezee bahati mwenyewe.
Kuna uzuri wa kutengeneza bahati yako mwenyewe kuliko kubahatika katika bahati nasibu ambazo unajaribu bila kuwa na uhakika kama wewe ndiye utakayebahatika au la. Unapojibahatisha mwenyewe unakua umejiandaa kupokea matokeo ambayo umekusudia yatatokea na ikiwa kama ulivyopanga inakuwa rahisi kulinda na kuongeza mafanikio yale ili uende kiwango cha juu zaidi. Tofauti na bahati nasibu ambazo mara nyingi ukishabahatika unachanganyikiwa kwa sababu ni kitu ambacho kimekuja kwa kushtukiza tu. Kukikuza pia ni kazi ngumu kwa sababu sio wewe uliyekitafuta. Simaanishi kuwa hutakiwi kupata bahati nasibu, maana yangu ni kwamba huwezi kujenga maisha unayoyataka kwa kutegemea kua kuna siku utabahatika na baada ya kufanya hivyo basi ndoto zako zitatimia.
Ili uweze kufikia kiwango cha mafanikio unachohitaji ni muhimu sana kuwa na nidhamu binafsi. Kama maisha yangekuwa ni aina fulani ya mlo mzuri, basi ningeweza kusema kuwa nidhamu ni kiungo muhimu sana ambacho kinafanya chakula hicho kiwe na ladha hiyo tamu. Ni vigumu sana kupanga shughuli na kuitimiza kwa wakati kama hauna nidhamu binafsi. Unaweza kujikuta hata kuchaji simu tu huwezi na unalalamika kuwa umeishiwa chaji umeme ukikatika na simu ulikua nayo muda wote na muda wote huo ulikua unawaza kuichaji , lakini kwa kutokua na nidhamu binafsi umejikuta unaendelea na mambo mengine yasiyo ya muhimu zaidi kwa wakati huo na kuacha kufanya mambo ya muhimu. Huu ni mfano mdogo tu wa namna ambavyo watu wengi wanashindwa kuwa na nidhamu katika maisha ya kila siku.
Ukisoma makala hizi, nakusihi jitahidi kuzipa nafasi katika akili yako ili uweze kukumbuka. Wakati hali ya kujisahaulisha, uvivu na kuahirisha vinapokuandama jitahidi ukumbuke baadhi ya vipengele ambavyo vitakusaidia kukupa nguvu ya kufanya shughuli ulizopangilia ambazo zitakusaidia kufikia kiwango cha mafanikio unachohitaji.
MWANDISHI: ESTHER NGULWA 
MAWASILIANO: 0767 900 110 / 0714 900 110 
Whatsaap: 0652 025244 
Facebook 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni